KARIBU KATIKA BLOG YAKO, UNARUHUSIWA KUTOA MAWAZO YAKO YATAKAYOJENGA

KATIBA MPYA

click hapa kudownload muswada wa sheria ya katiba

download katiba ya Tanzania

MAPENDEKEZO JUU YA MUSWADA WA SHERIA YA MABADILIKO YA KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, 2011

Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania, Deu Kibamba (kulia) akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA.
JUKWAA la Katiba Tanzania, linapenda kuwasilisha mapendekezo ya wananchi juu ya Muswada wa Sheria ya kuweka utaratibu wa mabadiliko ya Katiba Tanzania kama ifuatavyo. Maoni haya ni matokeo ya uchambuzi wa JUKWAA LA KATIBA TANZANIA wa maoni yaliyokusanywa kutoka kwa watanzania walioshiriki midahalo, semina, makongamano na mahojiano mbalimbali yaliyoandaliwa na JUKWAA LA KATIBA TANZANIA, asasi wanachama wake na makundi mengine ya Kijamamii tangu muswada wa Sheria ya Mapitio ya Katiba wa mwaka 2011 ulipotoka na kusomwa bungeni mwezi Aprili mwaka huu. Uchambuzi huu pia unahusu Muswada Mpya wa Sheria ya Mapitio ya Katiba, 2011 uliochapishwa katika gazeti la serikali Nambari 41 vol 92 la 14 October 2011.
Jukwaa la Katiba Tanzania linatambua juhudi ambazo zimefanywa na serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria za Serikali (CPD) na kwa kuweza kuzingatia baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa na wananchi wa Tanzania Bara na Zanzibar kuanzia Mwezi April, 2011 pale Muswada wa awali uliposomwa kwa mara ya Kwanza ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila mafanikio na ukaondolewa rasmi kwenye mchakato wa kusomwa bungeni mpaka ukaandikwe upya, tena kwa Kiswahili. Ni dhahiri kuwa yapo mambo ambayo angalau yameweza kubadilika kulingana na maoni yaliyotolewa na wasomi, wataalam na wananchi juu ya Muswada wa mwezi Aprili.
Hata hivyo, Inasikitisha kuwa kumekuwa na kusuasua katika kuukamilisha tena Muswada huu kwa ajili ya kuwasilishwa tena Bungeni. Ikumbukwe kuwa Muswada huu Mpya awali ulipangwa kuwasilishwa katika Mkutano wa Bajeti uliokamilika mwezi Agosti, 2011. Ni kutokana na kusuasua kwa ukamilishaji wa Muswada ndipo Bunge likaamua kufuta ratiba ya kujadili Muswada mwishoni mwa Mkutano wa Bajeti. Hata katika awamu hii, Muswaada umecheleweshwa sana kuchapishwa katika gazeti la serikali na kunyima fursa ya wananchi kuuona, kuuchambua na kuujadili, kabla kwenda Bungeni kwenda kusomwa kwa mara ya Kwanza. Ikumbukwe kuwa ilipendekezwa na wananchi wengi kuwa Muswada Mpya ujadiliwe si tu katika vituo vitatu vya Dar es Salaam, Dodoma na Zanzibar bali angalau kuwe na kituo cha Kujadili Muswada katika kila Mkoa. Hili nalo limeshindikana.
Kutokana na mambo yaliyojitokeza katika maandalizi ya Muswada huu mpya, na kwa kuzingatia maudhui yaliyomo katika Muswada wenyewe, JUKWAA LA KATIBA TANZANIA tuna Maoni yafuatayo:
Licha ya juhudi zilizofanywa na Serikali kuandaa Muswada huu, Jukwaa la Katiba Tanzania bado linasikitishwa na kitendo cha Serikali kuchelewesha kutoa na kusambaza Muswada kwa umma ndani ya muda wa kutosha kuwezesha wananchi walio wengi kupata fursa ya kushiriki majadiliano ya kina na kutoa maoni yao juu ya (kuhusiana na) maudhui ya Muswada kabla haujawasilishwa rasmi Bungeni. Tunatoa rai kuwa Muswada huu ni wa Katiba ya Watanzania katika Jamhuri yote ya Mungano wa Tanzania na hauwezi kuendelea kupitishwa bila ridhaa pana ya Watanzania.
Muswada kama huu uliwasilishwa na kukataliwa Bungeni katika kikao chake cha Aprili, 2011. Kwa mantiki hiyo muswada huu wa sasa ni mpya na hivyo ungetarajiwa kusomwa kwa mara ya kwanza Bungeni mwezi huu. Hivyo basi, pendekezo kuwa mswada huu ukiwasilishwa Bungeni utakuwa ukisomwa kwa mara ya pili na ya tatu ni upotoshaji. Muswada huu ni mpya kwa hiyo unatakiwa ukiwasilishwa Bungeni kwa mara ya kwanza. Tofauti ya Muswada kusomwa kwa mara ya kwanza na mara ya pili ni kwamba ukisomwa kwa mara ya kwanza kuna fursa ya wananchi kutoa maoni yao wakati ukisomwa kwa mara ya pili basi hakuna ulazima wa fursa yaWananchi kutoa maoni yao. Kitaalam, Muswada huu ulisomwa Bungeni kwa mara ya kwanza mwezi Aprili bila mafanikio na hauwezi kuletwa kwa ajili ya kusomwa kwa mara ya pili kana kwamba ulisomwa wa mafanikio.
Jina la Muswada bado ni tatizo na halishabihiani na maudhui makuu ya Muswada na lengo la tunachotaka kufanya kama nchi; huu si Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba bali Muswada wa Sheria ya Kuweka utaratibu, mchakato na vyombo vitakavyohusika katika kuandika Katiba Mpya Tanzania. Jina lake la sasa ni batili .Tunapendekeza kuwa Jina la Muswada huu liwe: MUSWADA WA SHERIA YA KUWEKA UTARATIBU NA VYOMBO VYA KURATIBU MCHAKATO WA KUPATA KATIBA MPYA TANZANIA. Hii itasomeka kwa Kiingereza kama – TANZANIA CONSTITUTION MAKING PROCESS BILL, 2011.
Kuna vipengele vingi vinavyoonyesha Serikali kukosa umakini katika kuandaa Muswada huu. Kwa mfano, mapendekezo kuwa Bunge Maalum la Katiba litaundwa na wajumbe wanaojumuisha wabunge wote wa Bunge la Tanzania na wawakilishi wote wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar na halafu kuongeza wajumbe wa nyongeza kuwa ni pamoja na Waziri wa Sheria na Katiba na Mwanasheria Mkuu wa serikali ni marudio yasiyo na sababu ya msingi. Kwa mfumo wetu, Waziri tayari ni Mbunge. Hii inaonyesha kuwa imechukuliwa kutoka katika nchi ambayo mfumo wake unaruhusu kuwa na Mawaziri wasio wabunge. Vivyohivyo, kwa wadhifa wake, Mwanasheria Mkuu wa Serikali tayari ni Mbunge. Na hii ni kwa pande zote za Muungano.
Kwa mwitikio na maudhui yake, Muswada huu unadhihirisha kuwa Serikali bado ina mtazamo kuwa inaandika Katiba ya dola (yake). Ukweli ni kuwa katika suala hili Serikali inapaswa kutambua kuwa ni mdau kama wadau wengine ila mwenye jukumu la kuwezesha wananchi kuandika Katiba ya Nchi yao. Kuendelelea kufanya mambo kwa usiri na vificho hakutaleta tija yoyote katika mchakato huu muhimu wa Kuandika KATIBA YA WATANZANIA.
Pamoja na vigezo vingine muhimu, Katiba ya Nchi sharti ibainishe kuwa ‘waraka wa kisiasa’ pia, lakini mapendekezo mengi yaliyomo kwenye Muswada huu yanaonesha kuwa Katiba itakayoandaliwa, kama ilivyo ya sasa, itakuwa ‘waraka wa kisheria’ na ‘waraka wa kiutawala’ tu (mamlaka makubwa ya Rais ni kielelezo). Sifa ya Katiba kama muafaka wa kitaifa na kijamii unaoleta maridhiano inakosekana katika Muswada huu. Endapo dalili za kukosekana kwa muafaka wa Kitaifa na Kijamii zitaanza kujionyesha sasa, kunaweza kutokea mgawanyiko mkubwa huko tuendako.
Muswada haujaweka lengo kuu la kuanzishwa kwa mchakato wa kuandika Katiba mpya. Hili ndio tatizo kuu la Muswada wenyewe na JUKWAA LA KATIBA TANZANIA hatutapitisha Muswada usiolenga kuandika Katiba Mpya. Kwetu sisi, Viraka katika katiba iliyopo na tunaona kuwa itakuwa ni kupoteza muda na rasilimali kuanzisha Mchakato utakaoishia kuzaa marekebisho mengine Katiba Katiba ya Nchi. Ikumbukwe kuwa Katiba iliyopo ya Tanzania tayari imefanyiwa marekebisho mara kumi na nne (14) tangu mwaka 1977 pekee.
Kutokana na Maoni haya tunatoa mapendekezo yafuatayo:
Utolewe muda na fursa ya kutosha kwa wananchi kupata muswada na kuujadili kabla ya kuwasilishwa kwa majadiliano rasmi Bungeni. Ili hilo litokee, Muswada utamke kuwa unakwenda kusomwa kwa mara ya kwanza na kwamba baada ya kusomwa wiki ijayo, kitakachofuata ni Kamati ya Bunge kufika kila Mkoa kukusanya maoni ya Wananchi kuhusu Muswada huu muhimu. JUKWAA LA KATIBA TANZANIA tuko tayari kusaidia kuandaa Wananchi kwa ajili ya utoaji wa Maoni katika Kila Mkoa.
Jina la Muswada libadilishwe na kuwa “Muswada wa Sheria ya Kuweka Utaratibu, Mchakato na Vyombo vitakavyohusika katika Kuandika Katiba Mpya Tanzania”.
Serikali ioneshe umakini kwa kuondoa vipengele vyote vinavyobainisha kutoandaliwa kwa umakini kama ilivyoainishwa katika uchambuzi wetu wa Kina (ulioambatishwa).
Maudhui na mwitikio wa lugha ya Muswada vionyeshe na kubainisha kuwa wananchi wa Tanzania ndio wanaoandaa Katiba yao, siyo Serikali, hivyo, vifungu vyote vinavyoonesha Serikali kupora mamlaka ya raia wa Tanzania kuandaa Katiba yao wakiratibiwa na Serikali, vifutwe na/au kuhaririwa na kurekebishwa ili viakisi ukweli wa mambo na matarajio ya Wananchi wa Tanzania. Hii ni pamoja na kupunguza kabisa, mamlaka kadhaa ya Rais katika mchakato huu wa kuandaa Katiba mpya ya Tanzania. Kwa mfano, itakuwa ngumu kwa Rais kutoa hadidu za Rejea kwa Tume ya KATIBA. Hadidu za Rejea lazima ziwe sehemu ya Muswada huu. Pia, itakuwa ngumu kwa Rais kuteua wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba. Iwekwe wazi kuwa wajumbe wa Bunge Maalum la KATIBA watachaguliwa na kupendekezwa na makundi wanakotokea kabla ya majina yao kuchapishwa katika gazeti la Serikali pamoja na yale ya wajumbe wengine kutoka Bunge la TANZANIA na Baraza la wawakilishi Zanzibar. Yatosha kabisa kwa Tume ya Katiba kupeleka majina hayo kwenye gazi la serikali. Ili kurahisisha jinsi ya upatikanaji wa wabunge MAALUM la Katiba, wachaguliwe wajumbe wawili (ke na me) kutoka kila wilaya, Tanzania Bara na Zanzibar ili kuwakilisha wilaya zao katika Bunge Maalum la Katiba.
Mfumo mzima na michakato ya kupata wasimamizi wa vyombo vya mamlaka ya mpito kuandaa Katiba mpya usiingizwe, kuchanganywa wala kumezwa na mfumo wa sasa wa kuendesha Serikali. Sheria hii iunde Tume Maalum ya uchaguzi kwa ajili ya kusimamia na kuendesha shughuli zote za upigaji kura za mchakato wa kuandaa katiba mpya. Sambamba na hilo, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lipewe jukumu la kusimamia kasi ya mchakato huu ili kuhakikisha kuwa hakuna kusuasua. Watendaji katika vyombo hivi waajiriwe kwa kufuata kanuni za ushindani na masharti ya utumishi wa umma.
Kwa kutimisha, tunapenda kutoa rai kwa watanzania wote kujitokeza na kuchangia kwa hali na mali katika Mchakato huu muhimu utakaopelekea watanzania kuandika Katiba yao. Muhimu zaidi, tunapenda kutoa wito kwa wasomi wa ngazi mbalimbali kujitokeza kusaidia kuhamasisha na kuelimisha umma wa Watanzania juu ya namna Katiba Mpya itakavyopatikana. Ni vema tukawezesha uelewa na uwazi ili wananchi wenyewe washiriki mchakato huu. Kwa upande wetu, JUKWAA LA KATIBA TANZANIA tuko mbioni kuunda na kutangaza jopo la wataalam wa masuala ya Katiba ambalo litakuwa na kazi ya kulishauri taifa kuhusu Mchakato huu kuanzia sasa mpaka tutakapopata Katiba Mpya ya Nchi. Tunawaomba mtakaoteuliwa kukubali kutumikia taifa letu kwa moyo na uadilifu Mkubwa.

0 comments:

Follow by Email

There was an error in this gadget
Html Free Code

wibiya widget